
Mwagane
IN SUMMARY
Mwagane, ambaye ana mwili uliojengeka kwa mazoezi, anacheza kwa kutumia akili na sifa ya kipekee aliyonayo ni uhodari wa kupiga mipira ya vichwa, kwani kati ya mabao sita aliyofunga, manne amefunga kwa staili hiyo. Anasema kipaji chake ni kwa sababu ya kujituma, bidii katika mazoezi na kumsikiliza kocha.
STRAIKA wa Mbeya City, Mwagane Yeya Mwanavyembe kwa sasa ni maarufu kutokana na kasi yake ya upachikaji mabao, anakumbukwa zaidi kwenye mechi yake ya kihistoria walipocheza na Azam FC, mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi, jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3, huku mabao yote ya Mbeya City yakifungwa Mwagane na kuondoka na mpira.
Mwagane, ambaye ana mwili uliojengeka kwa mazoezi, anacheza kwa kutumia akili na sifa ya kipekee aliyonayo ni uhodari wa kupiga mipira ya vichwa, kwani kati ya mabao sita aliyofunga, manne amefunga kwa staili hiyo. Anasema kipaji chake ni kwa sababu ya kujituma, bidii katika mazoezi na kumsikiliza kocha.
“Unajua kila kitu hupangwa na Mungu, malengo yangu ni kucheza mpira mzuri hadi kufikia kiwango cha kimataifa, nafahamu matunda ya kujituma ni mafanikio, nami katika hili sitaki kufanya makosa kabisa,” anaeleza Mwagane.
Mwagane aliitwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Young Future Taifa Stars, kilichocheza na Taifa Stars Jumatano iliyopita lakini hakucheza kwa sababu alikuwa anaumwa nyonga ya kushoto.
Anasema: “Awali sikutarajia kama siku moja naweza kushindana na wachezaji wengine wenye majina makubwa. Au kuchezea dhidi ya timu kubwa kama za Simba na Yanga, lakini pia sikutarajia kama siku moja naweza kuchezea timu ya Taifa, sitabweteka, naangalia mbele tu ili kuona nafanikiwa zaidi. Uzuri najitambua na najua ninachotakiwa kufanya ili kwenda sawa na nidhamu ya mpira.
“Najua baadhi ya vitu ambavyo vinawapoteza wachezaji wengi ni ulevi, uasherati, kutokulala mapema na nidhamu mbaya, kwangu mimi hivyo havina nafasi kabisa.
“Na nimejipanga vizuri kuanza mzunguko wa pili, nataka kuweka ushindani kwa wafungaji nimalize mfungaji bora kwa ajili yangu na timu yangu. Sikuweza kwenda na kasi ya mabao mzunguko wa kwanza kwa sababu ya kuwa majeruhi,’’ anasema Mwagane ambaye hakucheza mechi tatu.
Anaipenda Yanga
“Kama mchezaji nina mapenzi ya dhati na Mbeya City ingawa zamani nilikuwa naipenda Yanga,” anasema Mwagane mfungaji wa bao pekee la Mbeya City walipotoka sare ya bao 1-1 na Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
“Familia nyumbani hasa baba (Mzee Yeya Mwanavyembe) ni shabiki na mpenzi wa Yanga. Upenzi wake ulituambukiza sisi watoto wote, Yanga iliposhinda mechi zake nyumbani ilikuwa furaha tupu.
“Lakini sasa mapenzi yote ni Mbeya City, naipenda kwa moyo wangu wote na si Yanga tena kwa sababu naichezea Mbeya City hivyo nipo kikazi zaidi.
“Nilipoifunga Yanga mechi ya mzunguko wa kwanza, mzee nyumbani alichukia sana na ilipita kama mwezi hivi hatukuwa na maelewano mazuri. Lakini baadaye nilimwelekeza kuwa pale nipo kikazi lazima niwafunge ili kuisaidia timu yangu, nashukuru Mungu baada ya muda alinielewa.
Akizungumzia mafanikio ya Mbeya City, Mwagane anasema: “Maandalizi ushirikiano na morali wa wachezaji. Kila mchezaji ana uchungu na timu kwa sababu ni ya nyumbani na naichukulia kama yangu.”
“Hata upenzi wa mashabiki uliopo ni kwa sababu sehemu kubwa ya wachezaji waliopo, wanatoka kwenye jijini lile la Mbeya karibu kila wilaya ina mchezaji Mbeya City,” anasema.
“Hata hivyo tuna malengo tangu mwanzo, wapo waliokuwa wanatukatisha tamaa kwa sababu ya ugeni lakini nawahakikishia hakuna kitu kama hicho, tunataka kuweka historia.
“Tuna kila sababu, uongozi unatujali, tuna kocha mzuri (Mwambusi) kwa hiyo sioni cha kuturudisha nyuma,” anasisitiza. Ualimu na uchezaji
Mwagane anafafanua kuwa, maisha yake ya kila siku yanategemea kipato cha kazi yake ya ualimu, anafundisha Shule ya Sekondari ya Iduda iliyopo Uyole, Mbeya na kwenye soka anapata posho tu.
Awali wanafunzi waliandamana kwa ajili ya kukosa masomo kwani alikuwa peke yake mwalimu wa masomo ya biashara, lakini kwa sasa wameongezwa walimu wengine wawili.
“Mimi ni mtumishi wa Serikali, ni mwalimu kazi yangu ipo chini ya Mkurugenzi wa Manispaa na Mbeya City ni timu ya manispaa kwa hiyo hakuna utata, “anasema Mwagane aliyekuwa Waziri wa Michezo alipokuwa anasoma Chuo cha Ualimu, Kasulu TTC, Kigoma.
“Nacheza mpira kwa mapenzi na ni kama najitolea, pesa ninayoipata hapa ni posho tu na marupurupu mengine timu inaposafiri. Kama ningelipwa hapa, ingekuwa mara mbili jambo ambalo lisingewezekana lakini pia ingekuwa naichezea klabu nyingine ambayo haihusiani na manispaa, nisingeruhusiwa, hapa nina ruhusa kwa barua maalumu.”
Akizungumzia kujigawa kwake shule na uchezaji anasema: “Awali nilikuwa nakwenda mazoezini na baadaye shule ilikuwa lazima watoto wasome, ilinisumbua nilikuwa nachoka sana. Kuna wakati wanafunzi walikuwa wanakosa masomo wakaandamana lakini kwa sasa nashukuru, wameongezwa walimu wengine wa biashara.”
Mwagane pia alizungumzia iwapo Yanga, Simba au Azam zitamtaka: “Nitaangalia kwanza jinsi tutakavyozungumza, kama tutakubaliana mambo ya msingi naweza kushawishika. “Unaweza kukubali ofa kubwa ambayo ikakunufaisha kwa muda mfupi miaka miwili na baadaye ukaanza kuhangaika, akili yangu sasa ni kuisaidia Mbeya City klabu ambayo nina uchungu nayo na napenda kwa moyo wote kuhakikisha inafikia malengo, likifanikiwa hilo nasi tutafanikiwa,”anasema.
0 comments:
Post a Comment