IN SUMMARY

Pamoja na pongezi hizo, Makamba alitoa tahadhari akisema kwamba Mbeya City si klabu ya kwanza kutoka Mbeya iliyoweza kuwa tishio katika soka la Tanzania, akazitolea mfano Mecco na Tukuyu Stars.


IJUMAA iliyopita wakati wa utoaji wa tuzo za Mwanaspoti Bora wa Soka 2012/13 kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba aliizungumzia Klabu ya Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Bara.


Makamba alipongeza timu hiyo kwa juhudi ilizozifanya katika Ligi Kuu Bara ambayo kwa sasa ipo katika mapumziko baada ya mzunguko wa kwanza kukamilika.


Pamoja na pongezi hizo, Makamba alitoa tahadhari akisema kwamba Mbeya City si klabu ya kwanza kutoka Mbeya iliyoweza kuwa tishio katika soka la Tanzania, akazitolea mfano Mecco na Tukuyu Stars.

Tunaweza kusema kwamba Tukuyu na Mecco na hata Prisons zilikuwa tishio kuliko Mbeya City ambayo makali yake yameonekana mzunguko wa kwanza na hatujui itakuwaje katika mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza Januari 25 mwakani.

Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana tunatoa tahadhari kwa viongozi wa Mbeya City kutovimba vichwa na kujiona wamepiga hatua kubwa sana kama vile hakuna timu yoyote kutoka Mbeya iliyowahi kufanya kama wao. Mecco na Tukuyu si tu kwamba zilivitetemesha vinavyoitwa vigogo vya soka nchini bali Tukuyu ilifikia hatua ya kutwaa taji la ligi mwaka 1986 ambalo kwa Mbeya City hakuna mwenye uhakika kama timu hiyo itaweza kufanya hivyo.

Ni hivi karibuni tu Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni naye alitahadharisha akisema kwamba Mbeya City inayosifiwa hii leo inaweza kuyeyuka kimiujiza katika soka la Bongo.

Na ingawa hakwenda mbali lakini kubwa alilozungumzia ni fitna za soka ambazo zinaweza kuikwaza timu hiyo.


Hata hivyo jambo la msingi kwa viongozi na wachezaji wa timu hiyo ni kusimama imara na kuhakikisha kuwa misingi yote ya soka inasimamiwa katika kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana katika timu hiyo yanakuwa ya kudumu na si ya muda mfupi.

Tumekuwa tukisikia suala la timu hiyo kutokuwa tayari kuuza wachezaji wake hususan katika klabu za Yanga na Simba, kwetu sisi tunadhani hilo si suluhisho pekee badala yake ni vyema uongozi ukawa na mfumo endelevu wa kuinua vipaji.

Tunasema hivyo kwa sababu ni vigumu kwa klabu inayotaka mchezaji kwa dau kubwa halafu mchezaji mwenyewe akawa tayari kuhama timu ikafanikiwa kumzuia, hili ni jambo gumu kimsingi hata kanuni zinazotawala soka hazikubaliani nalo.

Vilevile tukumbuke kwamba soka ni biashara hivyo huwezi kukataa biashara kubwa inapojitokeza na hasa inapofikia hatua mchezaji akawa ameshawishika na malipo makubwa, la msingi ni kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa katika suala hilo.

Kitakachoilinda na kuiokoa Mbeya City ni mfumo mzuri wa kuibua vipaji mkoani Mbeya na si kuwazuia baadhi ya wachezaji kwenda Yanga, Simba au hata nje ya nchi pale watakapoona kwamba huko kuna maslahi kuzidi yale ya Mbeya City.

0 comments:

Post a Comment

    Blogger news

    Blogroll

    Pages

    About