By EDO KUMWEMBE,MWANASPOTI 
IN SUMMARY
  • Joseph ‘Sepp’ Blatter na watu wachache wakachukua fungu lao kwa njia za panya kutoka kwa Waarabu na Warusi, kisha mapambano yakaanza. Watu waliokuwa wanaamini kuwa walikuwa na nafasi kubwa ya kupata nafasi mojawapo katika hizo mbili ni Waingereza
SHARE THIS STORY
 
RONALD Reagan, Rais wa zamani wa Marekani aliwahi kusema ‘Mabadiliko yote makubwa yanayotokea Marekani, huwa yanaanzia katika meza ya chakula cha jioni’. Usibishe sana. Alikuwa sahihi.
Hata katika soka, mabadiliko mengi au uamuzi mwingi unaofanyika huwa yanaanzia katika meza ya chakula cha jioni. Huwezi kuona kwa macho ya moja kwa moja jinsi mchezo unavyochezwa.
Jioni moja ya Septemba 2, 2010, Waarabu wa Qatar walipewa nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2022. Usiku huo huo, Warusi walipewa nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018.
Baada ya hapo watu wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa)  wakakumbatiana, wakaanza kutafuna firigisi na kushushia vileo vya bei mbaya kama vile Krug Clos d’Ambonnay, 1928 Krug, 1893 Veuve Clicquot na vinginevyo. Maisha yanataka nini zaidi?  Lakini kabla ya hapo nina uhakika watu wa Qatar na Warusi walifanya kazi kubwa kuhakikisha wanapata nafasi hizi. Kama alivyosema Reagan, mabadiliko makubwa yanaanzia katika meza ya chakula cha jioni. Ni lazima mazungumzo yao yalianzia katika meza ya chakula cha jioni sehemu fulani hivi.
Joseph ‘Sepp’ Blatter na watu wachache wakachukua fungu lao kwa njia za panya kutoka kwa Waarabu na Warusi, kisha mapambano yakaanza. Watu waliokuwa wanaamini kuwa walikuwa na nafasi kubwa ya kupata nafasi mojawapo katika hizo mbili ni Waingereza.
Tatizo kubwa Waingereza waliamini katika mkono mtupu. Hawakujua kama haulambwi. Wakapeleka wauza sura wawili maarufu katika kampeni zao, Prince Williams na David Beckham.
Warusi hawakupeleka sura nzuri. Sura ya kwanza ilikuwa mbaya sana. Sura ya Andriy Arshavin. Sura ya pili ilikuwa ni ya Roman Abramovich. Hii nayo ni sura mbaya nyingine, lakini ambayo katika akaunti yake ina Dola 13 bilioni. Unataka nini zaidi hapo? Wajumbe wote wakaipa Russia kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018.
Lakini sasa kuna kichekesho kinaendelea. Kila ukisoma magazeti ya Waingereza unaona wazi kwamba yamekazana kweli kweli kuhakikisha kwamba Qatar inaondolewa nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia kwa sababu Juni mwaka huo kutakuwa na joto la hatari.
Hili Kombe la Dunia lichezwe Qatar majira ya baridi kuna uwezekano mkubwa ikibidi ratiba za ligi kubwa Ulaya zikavurugika kwa sababu kipindi cha baridi kwao si Juni, ni Desemba. Waingereza wanaamini kwamba hawawezi kusubiri mpaka 2026 kuomba kuandaa Kombe la Dunia. Wanataka fitina ifanyike, Qatar iporwe haki ya uenyeji halafu na wao waangaliwe kwa sababu kwa sasa wana ligi maarufu zaidi duniani na miundombinu yao inaeleweka.
Hapa ndipo ninapocheka. Kila dakika ninayomuona Sepp Blatter akikazana kusema Qatar lazima iandae Kombe la Dunia ndipo ninapozidi kucheka. Wanafikiri huyu mzee ni mjinga? Wanafikiri Fifa ni wajinga?
Fifa ni nchi ambayo haina serikali wala dola. Inaendeshwa kihuni tu. Tayari kina Blatter washapewa fungu lao na Qatar muda mrefu na sasa wanawacheka tu Waingereza. Wameshapewa fungu lao muda mrefu na akina Abramovich na wanawacheka tu Waingereza.
Ndivyo Fifa ilivyo. Unadhani kila kitu kinakwenda bure? Unadhani hata Afrika Kusini ilipewa bure bure kuandaa Kombe la Dunia? Kuna mambo yanaanzia katika meza ya chakula cha jioni. Haya ndiyo ambayo hayafahamiki kwa wengi.
Categories:

0 comments:

Post a Comment

    Blogger news

    Blogroll

    Pages

    About