
WAYNE ROONEY; Kuzaliwa: Oktoba 24, 1985 Mahali: Liverpool, England Urefu: Futi 5 inchi 9 Klabu: Manchester Utd Nafasi: Mshambuliaji Jezi: Namba 10 Taifa: England
IN SUMMARY
Wapo wanasoka wengi wanaojiiba na kuvuta sigara kwa siri:
LONDON, ENGLAND
WAKATI watu wa fani nyingine wakiendelea kuburudika na sigara kama kawaida ingawa wanaweka afya zao hatarini, wanasoka wanaonekana kama vile wamepigwa marufuku kabisa kutumia kiburudisho hicho.
Hata hivyo, wapo wanasoka wengi wanaojiiba na kuvuta sigara kwa siri.
Wayne Rooney
Mara kadhaa Rooney ameonekana akiwa na sigara mdomoni hasa wakati akiwa mapumzikoni na mkewe Coleen. Kitendo hicho kilikuwa kinamchukiza zaidi kocha wake wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, hasa wakati Rooney alipopigwa picha akivuta sigara wakati yupo mapumzikoni Las Vegas, Marekani, miaka miwili iliyopita.
Mesut Ozil
Ni wazi kwamba sigara hazijaathiri kasi wala uwezo wa Mesut Ozil. Mara kadhaa ameonekana akiwa na sigara mdomoni akiwa amejipumzisha na washikaji zake katika boti.
Hata hivyo kasi yake bado iko pale pale kwa saa. Ameingia Arsenal na kasi kubwa akiwa amefunga bao moja na kutoa pasi za mwisho tano katika mechi zake tano za mwanzo za Arsenal. Ozil vile vile alikimbia kilomita 11.63 katika ushindi wa Arsenal dhidi ya Napoli katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akiwa mchezaji wa tatu Arsenal kwa kukimbia kilomita nyingi zaidi kwenye pambano hilo.
Laurent Koscielny
Staa mwingine wa Arsenal ambaye ni mvutaji hasa achilia mbali Ozil na Jack Wilshere. Huyu amewahi kupigwa picha akiwa katika gari huku mkononi akiwa na paketi ya sigara. Hata hivyo kwa sasa bado ana kasi yake ile ile uwanjani.
Dimitar Berbatov
Ukiingia mitandaoni utakutana na picha nzuri ya Dimitar Berbatov. Staa huyu kutoka Ulaya Mashariki katika nchi ya Bulgaria, ni mvuta sigara mzuri ambaye hafai kuwa mfano kwa watoto wanaotaka kucheza soka
Zinedine Zidane
Alikuwa ana kila kitu katika soka. Uwezo wa kumiliki mpira, kupiga pasi, kupiga chenga na kila ukijuacho katika soka. Lakini kumbe staa huyo wa zamani wa Ufaransa na Real Madrid, pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kuimiliki sigara mdomoni mwake.
Mwaka 2006, alikuwa ameminya kando ya hoteli ya timu ya taifa ya Ufaransa akijivutia sigara zake wakati Ufaransa ikijiandaa kuchuana na Ureno katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Ujerumani.
Mario Balotelli
Kocha wa zamani wa Inter Milan, Jose Mourinho, aliwahi kusema kuwa ni vigumu sana kufanya kazi ya kumwongoza Super Mario Balotelli. Inawezekana alikuwa sahihi. Unahitaji kuhimili vishindo vyake na kimoja ni tabia yake ya uvutaji sigara.
Mara kadhaa staa huyo wa kimataifa wa Italia, alipigwa picha akionekana anafurahia fegi zake. Kocha wa zamani wa Manchester City, Roberto Mancini, ambaye alikuwa kipenzi kikubwa cha Balotelli, mara kadhaa alionekana kukerwa na kitendo cha Balotelli kuvuta sigara ovyo.
“Ni vizuri kama akiamua kuacha kuvuta sigara. Lakini kama akivuta sigara 10 kwa siku na kufunga mabao mawili kila mechi basi bora aendelee,” alisema Mancini akiliambia Gazeti la Daily Mirror la Uingereza mwaka jana.
Lionel Messi
Hauwezi kuamini. Katika upole wake wote ilidhaniwa kuwa Messi asingefikiriwa kuwamo katika orodha hii.
Lakini ipo picha inayomwonyesha Messi akiwa ufukweni huku akiwa ameiweka vyema sigara yake mdomoni. Mbaya zaidi, wachezaji wa Barcelona wanatumika katika kampeni ya kuzuia uvutaji wa sigara nchini Hispania.
Diego Maradona
Wengine wote wanavuta sigara ndogo. Lakini mkongwe huyu wa soka la Argentina huwa anavuta sigara kubwa maarufu kwa jina la Cuban Cigar
Mara nyingi akiwa mapumzikoni, Maradona ambaye amewahi kukumbwa na kashfa ya kutumia dawa za kulevya, amepigwa picha akiwa na sigara hiyo kwa raha zake. Ni mfano mbaya kwa wanasoka chipukizi duniani kote.
Jack Wilshere
Ndiye mwanasoka wa karibuni zaidi kushikwa akitumia fegi. Haishangazi kuona kiwango chake cha msimu huu kimefunikwa na Aaaron Ramseyn pamoja na mastaa wapya waliotua Arsenal akina Mesut Ozil na Mathieu Flamini.
Wilshere alishikwa akivuta sigara huku akiwa amezungukwa na wasichana katika klabu moja ya usiku jijini London. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, alionekana kukerwa na kitendo hicho cha Wilshere kiasi cha kuhitaji kuzungumza naye.
Hata hivyo katika pambano lililofuata baada ya kashfa hiyo, Wilshere alifunga bao dhidi ya West Brom na kuzua furaha kubwa kutoka kwa mashabiki wa Arsenal waliokuwa wanaimba ‘Jack Wilshere anavuta sigara kila anapojisikia’.
Socrates
Mchawi wa soka wa zamani wa Brazil. Licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa soka uwanjani, lakini Socrates alikuwa mchezaji mwenye akili nyingi uwanjani.
Alikuwa ni daktari akiwa amesomea katika Chuo cha Faculdade de Medicina de Ribeirao Pretona na aliwashangaza wengi kwa kujipatia shahada yake angali akipiga soka.
Hata hivyo, usomi wake haukumsaidia Socrates katika kujiepusha na maisha ya uvutaji sigara na unywaji wa pombe.
0 comments:
Post a Comment