
Barkley alizaliwa Desemba 5, 1993 katika eneo la Wavertree jijini Liverpool ambayo ni makazi ya klabu mbili kubwa za watani wa jadi wa Merseyside, Liverpool na Everton.
SHARE THIS STORY
EVERTON imerudi tena katika makali yake ya kusumbua vigogo na katikati ya uwanja katika dimba lao wanajivunia kinda mdogo tu anayeitwa, Ross Barkley. Kwa nyakati tofauti, kinda huyo amefanikiwa kuwafunika mastaa wa timu kubwa za England kila anapokutana nao.
Azaliwa Liverpool, afuata nyayo za Rooney
Barkley alizaliwa Desemba 5, 1993 katika eneo la Wavertree jijini Liverpool ambayo ni makazi ya klabu mbili kubwa za watani wa jadi wa Merseyside, Liverpool na Everton.
Wachezaji wengi chipukizi wa jiji hili kama Michael Owen, Jamie Carragher, Wayne Rooney na wengineo huangukia katika timu moja kati ya Liverpool au Everton. Barkley aliangukia katika kambi ya vijana ya Everton akiwa na umri wa miaka 11.
Kuanzia hapo alitamba katika timu ya vijana huku akipata faida kubwa kutokana na kuwa na umbo kubwa kuliko wenzake. Alitajwa katika kikosi cha kwanza mwanzoni mwa msimu wa 2010–11 na alitazamiwa kucheza mechi ya kwanza ya ligi msimu huo, lakini kwa bahati mbaya akavunjika mguu mara tatu baada ya kugongana na beki wa Liverpool, Andre Wisdom katika pambano la wachezaji walio chini ya umri wa miaka 19. Ilikuwa Oktoba 2010.
Aumia, Moyes amlipia likizo yake
Kocha wa Everton wakati huo, David Moyes, alikuwa anampenda Barkley kupindukia na alikuwa anamlinda kila mahali. Kutokana na kukulia katika familia isiyo na kipato kikubwa, Moyes, alilazimika kumlipia Barkley pesa ya likizo ili yeye na familia yake nzima waende Tenerife kupumzika
“Wiki moja baada ya kuumia nilirudi nyumbani na alikuja kuniona kwetu Wavertree. Watoto wengi walijaa nyumbani waliposikia kuwa David Moyes alikuwa ndani ya nyumba yetu. Hilo lilikuwa jambo muhimu kwangu. Alikaa na sisi na kumwambia mama yetu kwamba ningepona. Wiki moja kabla madaktari walikuwa wananiambia kuwa maisha yangu ya soka huenda yamefika mwisho,” alisema Barkley.
Apona, atinga kikosi cha kwanza Alifanikiwa kupona na kujiunga katika mazoezi ya mwanzo wa msimu wa 2011–12. Wakati wa mazoezi hayo, staa wa zamani wa Everton, Tim Cahill, alisikika akisema kuwa Barkley alikuwa kinda mahiri zaidi aliyewahi kufanya kazi naye.
Alicheza mechi yake ya kwanza katika kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Queens Park Rangers na alitajwa kuwa mchezaji wa mechi. Baadaye, beki wa zamani wa Arsenal, Martin Keown, alisikika akisema kuwa Barkley angekuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea England. Alisaini mkataba wa miaka minne Desemba 2011.
0 comments:
Post a Comment