
Wachezaji wa Nigeria, wakifanya mazoezi yao kujiandaa na mechi yao hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa itakayofanyika jumatatu. Picha na AFP
Kwa ufupi
Haijawahi kuitokea Afrika kuingiza timu zaidi ya moja katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia.
Rio de Janeiro, Brazi. Ushiriki wa Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Brazil mwaka huu umekuwa wenye sura tofauti.
Ingawa Afrika inaweza kujivuna kwa kufanikiwa kuingiza timu mbili, Nigeria na Algeria kwenye hatua ya 16 bora, lakini ushiriki wa timu zake tano ulikuwa wa kusuasua. Katika baadhi ya nyakati, timu kadhaa zilikabiliwa na hatari ya nyota wake kususia fainali hizo kwa sababu ya madai ya fedha za posho na bonasi.
Kati ya timu tano zilizoshiriki, tatu zilikuwa na mizozo yaliyotokana na tatizo la upatikanaji wa fedha.
Mojawapo ya timu hizo, Ghana ilifikia mahali ambako uongozi wa nchi hiyo ulilazimika kusafirisha fedha kwa ndege maalum ya kukodi kwenda Brazil.
Nje ya mizozo hiyo ya fedha, nusura Afrika iingize timu tatu ambazo ni Nigeria, Algeria hata Ivory Coast ambayo ilitolewa kwa mkwaju wa penalti ya utata dakika ya mwisho dhidi ya Ugiriki.
Ni jambo ambalo halijawahi kuitokea Afrika miaka ya nyuma kuingiza timu zaidi ya moja katika hatua ya 16 bora.
Kiwango cha soka ambacho kimeonyeshwa na nchi za Afrika kimeridhisha wengi, jambo ambalo linawapa nafasi na jeuri ya kudai nyongeza ya washiriki kutoka timu tano za sasa katika miaka michache ijayo.
Mbali ya mafanikio hayo, lakini mizozo inayotokana na madai ya posho, bonasi, Afrika haina cha ziada cha kujivunia, kwani kabla ya fainali zinazoendelea nchini Brazil, timu tatu zilikuwa na mizozo, jambo ambalo limeathiri ushiriki wao, kama ambavyo imetokea kwa Ivory Coast, Ghana na Cameroon.
“Ni jambo linalotia doa mafanikio ya Afrika katika ulimwengu wa soka,” anaeleza Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, Jerome Valcke wakati akizungumzia madai ya wachezaji wa Ghana waliotishia kujitoa kwenye fainali za Kombe la Dunia kutokana na madai ya bonasi ambazo hazikuwa zimelipwa.
Ghana, ambayo iliishia robo fainali mwaka 2010, ilikuwa na wakati mgumu kiasi cha kulazimika kusafirisha fedha kwa ndege kuwatuliza wachezaji kabla ya kuivaa Ureno, mchezo ambao walifungwa mabao 2-1.
Kikosi cha Cameroon kiligoma kusafiri kwenda Brazil kwa madai ya posho na bonasi.
Mabingwa wa Afrika, Nigeria, siku chache kabla ya kuanza kwa fainali za mwaka 1998, waligomea mazoezi wakidai posho. Tatizo la malipo ya fedha kwa nchi za Afrika limekuwa tatizo na pia siyo jipya.
0 comments:
Post a Comment