

Yondani: Beki huyu wa Yanga mwenye miaka 29 anasema tuzo za Mwanaspoti zitaonyesha ufanisi wa mchezaji husika kwenye kazi na jinsi anavyokubalika kwenye jamii ya wanamichezo na amesifia kwamba ni ubunifu mzuri kwa Mwanaspoti unaofaa kuigwa ili kuongeza morali kwa wanamichezo.
By LASTECK ALFRED,MWANASPOTI (email the author)
Posted Alhamisi,Novemba7 2013 saa 10:37 AM
IN SUMMARY
Wachezaji watano waliofika fainali ni Kelvin Yondani, Amri Kiemba, Themi Felix, Haruna Niyonzima na Shomari Kapombe.
SHARE THIS STORYTweet
KILELE cha Tuzo za Mwanaspoti Bora wa Soka Tanzania 2013 zinafanyika kesho Ijumaa jioni kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Tuzo hizo zinashindanisha wachezaji waliofanya vizuri msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara.
Katika tuzo hizo kutakuwa na vipengele mbalimbali kama mchezaji chipukizi bora, mchezaji bora wa kike Tanzania, mfungaji bora, mchezaji bora Mtanzania anayecheza nje ya nchi, mchezaji bora wa kigeni anayecheza Tanzania na vipengele vingine vitakavyoshindaniwa.
Mashabiki wamekuwa wakipiga kura za kielektroniki wakati jopo lililosheheni wadau, wanamichezo, makocha na wataalamu mbalimbali wamekuwa wakifanya uratibu.
Wachezaji watano waliofika fainali ni Kelvin Yondani, Amri Kiemba, Themi Felix, Haruna Niyonzima na Shomari Kapombe.
Tuzo hizo zilizodhaminiwa na Kampuni ya Vodacom Tanzania, Clouds FM zimeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ambao ndio wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Wachezaji wote wamesema kuwa mashabiki ndio watakaoamua hatima yao. Jinsi ya kuwapigia kura ni kufungua sehemu ya kuandika ujumbe wa maneno kwenye simu yako, andika ujumbe mfupi unaoanza na neno KURA kisha jina la mchezaji unayempigia kura na tuma kwenda namba 15678. Atakayepata kura nyingi ndiye atakayekuwa mshindi hapo kesho.
YONDANI
Beki huyo wa Yanga mwenye miaka 29 anasema tuzo za Mwanaspoti zitaonyesha ufanisi wa mchezaji husika kwenye kazi na jinsi anavyokubalika kwenye jamii ya wanamichezo na amesifia kwamba ni ubunifu mzuri kwa Mwanaspoti unaofaa kuigwa ili kuongeza morali kwa wanamichezo.Anasema: “Kupitia Mwanaspoti na tuzo zake, utaweza kujua unafanyaje unapokuwa ndani na nje ya uwanja.”
Anasema kuwa haogopi lolote, zaidi anawaachia watu kupima yupi ni bora zaidi ya wengine na anaamini tuzo hizo zina maana kubwa kwake na watu wanaojua anachokifanya hivyo anamwomba Mungu ampe nafasi ya kushinda kwani wote anaoshindana nao ni wachezaji wa maana.
Yondani ameomba kwa kusema: “Najua wanajua uwezo wangu na wanajua kuwa Yondani anaweza, wanipe kura nishinde.”
HARUNA
Haruna Niyonzima anasema kuwa tuzo ni nzuri na amekuwa akizifuatilia lakini anafurahi kuwa zimeletwa kwa lengo la kuleta ushindani baina ya wachezaji.
“Tuzo za Mwanaspoti zitasaidia kuleta ushindani na pia kuleta ari kwa wachezaji kujituma na kucheza vizuri na hivyo wasifu wa mtu kupanda kipindi anapozipata,” anasema.
Niyonzima anasema kuwa kila mchezaji anayeshindania tuzo hizo ni mzuri lakini kila kitu kina watu wa kuamua hivyo wanaopiga kura wanajua ni sababu zipi watatumia kuchagua mshindi.
Kuhusu kura Niyonzima anasema: “Mashabiki na wapiga kura waangalie kwa umakini anayestahili kushinda na wasiwe na mapenzi tu, wampe mtu makini.”
THEMI
Themi Felix Buhaja ambaye ni straika wa Kagera Sugar anasema: “Cha kwanza nilichofurahia ni kuona jina langu miongoni mwa wale wanaoshindana kwenye fainali za tuzo hizo. Mwanaspoti imeandaa bonge la kitu, nitakuwa na furaha kama nitashinda kwani nitaendelea kuthibitisha ubora wangu nitakapokuwa uwanjani.”
Anasema kuwa anawaheshimu washindani wenzake kwani wao ni bora ndiyo maana wako kwenye hatua waliyopo. Themi anasema: “Naomba Watanzania, hii ni ya kwanza, najua wananipigia kura lakini sasa naomba wanipige zaidi nishinde.”
KAPOMBE
Shomari Kapombe ambaye alifanya vizuri na Simba msimu uliopita na sasa yupo kwenye klabu ya Klabu ya AS Cannes ya Ufaransa anasema: “Nakumbuka kabla sijaondoka Tanzania Mwanaspoti walikuwa tayari wameanza mchakato huu na baadaye nikaambiwa niko kwenye hatua ya tano bora hivyo nilifurahi sana.”
Kapombe alisema kuwa anaamini kila mchezaji anayeshindana tuzo hizo ni mzuri ndiyo maana yupo alipo kwa sasa. Beki huyo ameomba wadau wampigie kura na ana uhakika wa kufanya vizuri kwenye fainali hizo.
KIEMBA
Amri Kiemba, ni kiungo wa Simba anasema kuwa tuzo hizo zinalenga kuwasaidia wachezaji na kuwafanya wajitume zaidi: “Mwanaspoti imefanya kitu kizuri kuandaa tuzo hizo, hivyo tuwape sapoti ili waziandae mara kwa mara kwani mchezaji unapopewa tuzo ni heshima kubwa kuliko pesa unazolipwa na unazozitumia.
“Mawazo haya ya tuzo yaliyofanywa na Mwanaspoti yanahitaji kuungwa mkono na wasomaji na wapenzi wa soka ili Mwanaspoti washawishike kuzifanya kwa kila mwezi na si kila mwaka,” anasema Kiemba.
Kiungo huyo pia amesema kuwa ana changamoto kwenye tuzo hizo lakini anaamini kupitia wapenzi wa soka atashinda.” Licha ya changamoto za wale ninaoshindana nao, nafurahi niko mingoni mwa watano na nimepenya kwenye orodha ya wengi.”
Kiemba anasema: “Naomba mashabiki wanipigie kura, nitafurahi kupata heshima ya kuwa mchezaji wa kwanza kupata tuzo hizi pamoja na kuwa na rekodi ya heshima iliyotambua mchango wangu kwenye soka nchini.”
0 comments:
Post a Comment