Ni timu nne tu katika mzunguko huu wa kwanza wa Ligi Kuu zimeonyesha zina njaa ya ubingwa.
Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaelekea kuhitimishwa Alhamisi hii, ambapo baadhi ya timu shiriki zimeonyesha ushindani wa kweli huku zingine zikionekana kama washiriki tu na wasindikizaji.
Timu 14 zinashiriki Ligi Kuu msimu huu ambazo ni Azam FC, Yanga, Simba, Coastal Union, Mgambo Shooting, Oljoro JKT, Kagera Sugar na Ashanti United.
Nyingine ni Mtibwa Sugar, Mbeya City, Tanzania Prisons, JKT Ruvu, Ruvu Shooting na Rhino Rangers.
Hizi zifuatazo  zina njaa na fursa ya kutwaa ubingwa
Azam
Iliunza msimu huu kwa kusuasua kwani ilianza kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar, lakini ilibadilika kadri muda ulivyosonga na kuvuna matokeo mazuri yaliyoipaisha juu  katika msimamo wa ligi.
Azam ina fursa ya kutwaa ubingwa msimu huu kutokana na kuwa na kikosi kilichokamilika, pia inamaliza mzunguko wa kwanza ikiwa katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi.
Yanga
Haikuwa na wakati mzuri mwanzoni mwa msimu baada ya kuambulia sare mfululizo katika mechi zake tatu, hata hivyo taratibu ilianza kubadilika na mpaka sasa ipo katika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi.
Inaweza kutetea taji msimu huu kutokana na kuwa na kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji walioiva vizuri kila idara, hailazimiki kuongeza mchezaji wakati wa usajili wa dirisha dogo mwezi Januari.
Simba
Imekuwa na mwenendo wa kuvutia tangu mwanzoni mwa msimu huu baada ya kufanya vizuri katika mechi 11 ikiwa imeshinda tano na imetoka sare sita.
Simba inaweza kutwaa ubingwa msimu huu kutokana na kuundwa na wachezaji wengi vijana na wachache wakongwe kutoka ndani na nje ya nchi ingawa pia inatakiwa kuongeza wachezaji katika dirisha dogo hasa katika nafasi ya mabeki wa pembeni na ushambuliaji.
Mbeya City
Imeonyesha kiwango cha kuvutia mzunguko huu wa kwanza. City ina sababu ya kuibuka bingwa wa Ligi Kuu msimu huu kutokana na kuwa na kikosi chenye wachezaji wengi vijana waliofundishika.
Mazoezi  ya nguvu hasa milimani yamewasaidia vijana wa timu hiyo kuhimili mikikimikiki ya ligi kwani wamekuwa na nguvu na hawachoki dakika zote 90.
Hawana ulazima sana wa kuongeza wachezaji katika dirisha dogo la usajili ingawa wanashauriwa kuongeza mshambuliaji ili kuipa nguvu timu hiyo katika ufungaji wa mabao kwani wengi wanaofunga mabao mengi katika timu hiyo ni viungo na mawinga.
Hizi zinaleta ushindani ila hazina habari na ubingwa
Ruvu Shooting
Imedhihirisha ipo kwa ajili ya kushindana si kushiriki baada ya kushinda mechi tatu za mwanzo na wakati fulani kukalia kiti cha uongozi.
Shooting itafanya vizuri zaidi mzunguko wa pili na hata kutwaa ubingwa kama benchi lake la ufundi linaloongozwa na kocha Charles Mkwasa litaongeza nguvu katika safu yake ya ushambuliaji kwa kusajili mshambuliji mahiri atakayeshirikiana na Elias Maguli kwani safu yake ya ushambuliaji ilivyo hivi sasa haionyeshi kama inataka kutwaa ubingwa.
Kagera Sugar
Ni miongoni mwa timu zilizoonyesha kiwango kizuri na upinzani wa hali ya juu mzunguko huu wa kwanza wa ligi.
Benchi la ufundi la Kagera lililo chini ya kocha Jackson Mayanja linahitaji kufanya maboresho kidogo tu hasa katika safu yake ya ushambuliaji ili timu yao ifanye vizuri zaidi mzunguko wa pili na kuonyesha inataka kutwaa ubingwa.
Msimu uliopita ilionyesha soka la kiwango cha juu wakati huo ikiwa na kocha wa sasa wa Simba, Abdallah Kibaden na nusura ikamate nafasi ya tatu kwenye ligi kama si kuteleza katika mchezo wa mwisho.
Mtibwa Sugar
Imeonyesha ukomavu katika mzunguko huu wa kwanza, ingawa imekuwa haitabiriki katika matokeo na hivyo kuwa katika kundi ambazo hazina habari na ubingwa.
Kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wake wengi kumeidhoofisha timu  hiyo msimu huu ingawa pia kocha mkuu Mecky Mexime anatakiwa kuiangalia kwa jicho la tatu safu yake ya ulinzi kwani imeonekana kuyumba. Inaweza ikaleta ushindani mkubwa kwenye mzunguko wa pili na hata kukamata nafasi za juu kama itarekebisha kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza katika mzunguko wa kwanza, lakini hivi sasa haina habari na ubingwa.
Costal Union
Imeonyesha ushindani mzuri kwenye mzunguko huu wa kwanza. Coastal itafanya vizuri zaidi mzunguko wa pili kama benchi la ufundi la timu hiyo litaongeza makali ya safu yake ya ushambuliaji ambayo imeonekana kukosa umakini, pia kama benchi hilo la ufundi litakuwa na mfumo mzuri zaidi wa kutaumia nyota wengi ilionao.
Rhino Rangers
Timu hii ngeni kwenye Ligi Kuu ilikuwa na mwenendo mzuri katika mechi zake za awali, lakini ikajikuta ikipoteza mwelekeo kadri siku zilivyokwenda.
Rangers bado ina nafasi ya kufanya vizuri mzunguko wa pili kama benchi la ufundi la timu hiyo lililo chini ya Sebastian Nkoma litatumia kipindi cha usajili wa dirisha dogo kuongeza wachezaji kadhaa wenye uzoefu.
Ashanti United
Kama ilivyo kwa Rangers, pia Ashanti ni timu ngeni iliyoanza msimu huu kwa kusuasua baada ya kuchapwa mabao 5-1 na Yanga, lakini ilipevuka na kuanza kucheza soka la malengo na kuvuna ushindi katika baadhi ya mechi zake.
Ashanti itakuwa na wakati mzuri zaidi mzunguko wa pili kama benchi lake la ufundi linaloongozwa na Mbaraka Hassani litatumia kipindi cha usajili wa dirisha dogo kusajili wachezaji kadhaa mahiri wenye uzoefu kwa sababu hivi sasa ipo katika kundi ambalo halina habari na ubingwa.
Hazina habari ya ubingwa na zinahitaji mabadiliko makubwa
Tanzania Prisons
Ilionyesha kama itakuwa miongoni mwa timu zitakazotoa ushindani mkubwa msimu huu, lakini ukweli ni kwamba imeshindwa kuhimili vishindo na haichezi soka la malengo.
Zamani timu hiyo ilikuwa ikiogopwa na vigogo Simba na Yanga kila ilipokaribia kukutana nayo kwani ilikuwa ikisifika kuwa na aina ya wachezaji wenye nguvu na wanaojua soka, lakini siku za hivi sasa ina  wachezaji wa kawaida ambao hawaonyeshi ushindani wa kweli.
Mzunguko huu wa kwanza haikufanya vizuri, inahitaji mabadiliko makubwa kuweza kurejea katika ushindani mzunguko wa pili. Prisons inatakiwa kusajili wachezaji wenye uzoefu au kuwarudisha wazoefu wa timu hiyo iliyowatema hivi karibuni.
JKT Ruvu
Kati ya timu zilizokuwa zikisifika kwa soka safi tena la ushindani  misimu iliyopita ni JKT Ruvu, lakini msimu huu imepotea na haina ushindani tena.
Timu hiyo ilikuwa ikiogopwa na kila timu lakini sasa hivi timu zote zinazocheza na JKT Ruvu zinaona jambo la kawaida kwani haina tena makali.
Ilifanya vizuri katika mechi zake za mwanzo wa msimu na hata wakati fulani kukalia kiti cha uongozi, ghafla ikapoteza mwelekeo.
JKT Ruvu inahitaji mabadiliko makubwa katika kikosi chake.
JKT Mgambo
Imekuwa na mwenendo mbovu tangu mwanzoni mwa msimu mpaka sasa kwani ina wachezaji wa kiwango cha chini.
Mgambo inahitaji mabadiliko makubwa ili kuhakikisha inafanya vizuri mzunguko wa pili, inatakiwa kusajiliwa wachezaji wenye hadhi ya kucheza Ligi Kuu tofauti na ilionao sasa. Ikifanya hivyo inaweza ikabadilika mzunguko wa pili.
JKT Oljoro FC
Imeboronga tangu mwanzo wa msimu na ina hali mbaya kwani inashika nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi. Oljoro inahitaji mabadiliko kwani bila hivyo itashuka daraja. Oljoro ipo katika hali mbaya msimu huu kwani baadhi ya wachezaji wake walihamia timu nyingine na usajili uliofanywa kwa ajili ya msimu huu umeshindwa kuisaidia katika mzunguko wa kwanza kwa hiyo inahitaji mabadiliko makubwa ili ifanye vizuri katika mzunguko wa pili.


Categories:

0 comments:

Post a Comment

    Blogger news

    Blogroll

    Pages

    About