
Vijana wa Mbeya City walikuwa wa kwanza kulishambulia lango la Prisons na kuamsha vifijo kwa dakika tano mfululizo, lakini Prisons ilitulia na kuonyesha uzoefu wao.
IN SUMMARY
- Siku ya mechi, mashabiki wa timu hizo walianza kuingia uwanjani tangu saa 4:00 asubuhi huku matarumbeta yakisikika kuanzia alfajiri ya Jumanne na Mbeya City walionekana kutawala zaidi kwa mbwembwe za bendera, jezi, kofia na hata vitambaa vyenye rangi ya jezi ya timu yao.
MASHABIKI wa Mbeya City wameipongeza timu yao kwa kuifunga Prisons huku wakitamka kwa neno la Kinyakyusa; “Ndaga fijo” yaani ‘Asanteni sana’.
Jiji la Mbeya juzi Jumanne lilizizima kipekee baada ya timu mbili zenye maskani yake jijini hapa kuchuana katika Uwanja wa Sokoine ikiwa ni moja ya mechi za Ligi Kuu Bara huku vituko, tambo na mbwembwe za kila aina zikitawala.
Timu hizo ni za Mbeya City na Tanzania Prisons ambazo kwa sasa zimedhihirisha wazi kwamba ni timu zenye utani wa jadi mithili ya vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga.
Siku mbili kabla ya mechi hiyo, mitaa mbalimbali ya Jiji la Mbeya ilianza kutawaliwa na vituko vya mashabiki wa Mbeya City na waendesha bodaboda, magari na hata baiskeli walioonekana wakipeperusha bendera mitaa mbalimbali na nyingine wakazitundika juu ya miti ambayo rangi ya maua yake inafanana na rangi ya jezi za timu yao.
Kwa upande wa Prisons hakukuwa na mbwembwe za bendera nyingi licha ya kutundikwa eneo la gereza la Ruanda, lakini mashabiki, wachezaji, viongozi na baadhi ya wachezaji walitamba waziwazi wakisema wataishushia kipigo bila huruma timu hiyo.
Prisons walienda mbali zaidi kusisitiza wazi kwamba Mbeya City ni watoto na hawawezi kufurukuta kwani mtani wake alikuwa Tukuyu Stars, timu ambayo iliwika tangu mwaka 1986 hadi mwaka 2008 ilipoteremka daraja. Wachezaji wa zamani wa Prisons wakiongozwa na Samson Mwamanda walitamba kwenye mitandao ya kijamii kwamba Mbeya City haina lolote na ingeadhirika. Lakini mambo yakawa tofauti baada ya dakika 90 na wote wakaingia mitini.
Siku ya mechi, mashabiki wa timu hizo walianza kuingia uwanjani tangu saa 4:00 asubuhi huku matarumbeta yakisikika kuanzia alfajiri ya Jumanne na Mbeya City walionekana kutawala zaidi kwa mbwembwe za bendera, jezi, kofia na hata vitambaa vyenye rangi ya jezi ya timu yao. Prisons walijiamini sana na kwao maneno yalikuwa kidogo kwani walipania kushinda ili kulituliza jiji la Mbeya huku wakipata hamasa kutoka kwa Katibu Mkuu wao Mbarak Abdulwakil.
Uwanja wa Sokoine unaobeba mashabiki 20,000 ulianza kupumulia juu juu ilipotimu saa 9:00 alasiri wakati jukwaa la mashabiki wa Mbeya City lilikuwa limejaa watu waliojinakshi kwa vitu mbalimbali ikiwamo kujichora usoni na kichwani.
Kabla ya mechi kuanza, vituko viliendelea kwani vijana wa Mbeya City walionekana wakicheza ngoma na matarumbeta huku wakizunguka kutoka eneo lao hadi Jukwaa Kuu.
Mashabiki wa Prisons walipoona hayo nao wakiwa na matarumbeta waliamua kuzunguka hadi kwenye Jukwaa Kuu huku wakicheza kwa mbwembwe.
Mara ndege watatu aina ya njiwa, walionekana wakirukaruka kwa mbwembwe katikati ya uwanja jambo ambalo liliwaamsha mashabiki wengi kushangilia huku wengine wakishindwa kujua maana yake.
Hatimaye kabumbu lilianza kwa kasi saa 10:30 jioni chini ya mwamuzi Israel Nkongo aliyekuwa katikati, akisaidiwa na Samweli Mpenzu wa Arusha na Mohamed Mkono kutoka Tanga.
0 comments:
Post a Comment