YANGA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI, YAICHAPA JKT RUVU 4 - 0


Kikosi cha Young Africans kilichoanza leo dhidi ya JKT Ruvu






















Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Young Africans leo imekamata kiti cha uongozi baada ya kuendeleza wimbi la ushindi mfululizo kwa kuichapa timu ya Maafande wa jeshi la Kujenga Taifa nchini JKT Ruvu kutoka mkoani Pwani kwa mabao 4- 0 mchezo uliofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Kikosi cha mholanzi Ernie Brandts kiliingia uwanjani kwa lengo la kuhakikisha kinapata pointi 3 muhimu , jambo ambalo vijana wake walilitekeleza na kuwapa furaha washabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Yanga waliokwepo uwanjani kushuhudia mchezo huo.
 
Mshambuliaji Mrisho Ngassa aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 3 ya mchezo kwa shuti kali baada ya kuwatoka walinzi wa JKT Ruvu na kumtazama amekaa vipi mlinda mlango wa JKT Ruvu na kuukwamisha mpira wavuni.
 
Dakika ya 12 ya mchezo, Mrisho Ngassa tena aliwainua vitini mashabiki wa timu ya Young Africans baada ya kumalizia mpira ulipogwa na Saimon Msuva kabla ya kuwababatiza walinzi wa JKT Ruvu na kumkuta mfungaji ambaye aliukwamisha mpira wavuni kwa kichwa.
 
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, JKT Ruvu 0 - 2 Young Africans .
 
Kipindi cha pili cha mchezo kilianza kwa kasi na Young Africans kupata bao la tatu la mchezo dakika ya 47 kupitia kwa Oscar Joshua ambaye alikutana na mpira uliokolewa walinzi wa JKT na kumkuta mfungaji ambaye alifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na klabu ya Yanga miaka mitatu iliyopita.
 
Mabadiliko yaliyofanya na kocha mholanzi Ernie Brandts kuwaingiza Reliants Lusajo, Ibrahim Job na Jerson Tegete yaliongeza kasi na uwezo wa kumiliki mchezo kwani waliweza kucheza vizuri na kulilinda lango lao lisipatwe na madhara yoyote.
 
Dakika ya 89 Jerson Tegete aliipatia Yanga bao la nne la mwisho katika mchezo huo kufuatia migongeo ya Saimon Msuva na Ngassa kabla ya kumkuta Tegete akiwa peke yake na kuukwamisha mpira wavuni.
 
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, JKT Ruvu 0 - 4 Young Africans

Young Africans: 1.Dida, 2.Twite/Job, 3.Oscar, 4.Cannavaro 5.Yondani/Lusajio, 6.Chuji 7.Msuva 8.Domayo, 9.Kavumbagu/Tegete, 10.Ngassa, 11.Kiiza

source: http://www.youngafricans.co.tz

Thursday, October 31, 2013

MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA KUMENYANA BONANZA LA NANI MTANI JEMBE SONGEA.

Na Mwandishi Wetu

Mashabiki wa Simba na Yanga mjini Songea watamenyana vikali katika michezo mbalimbali kupitia bonanza maalum la Nani Mtani Jembe lililoandaliwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager litakalofanyika uwanja wa Maji Maji mjini Songea Jumapili wikendi hii.

Mratibu wa bonanza hilo Amadeus Kalumuna, amesema kuwa michezo mbalimbali ikiwemo soka bonanza la wachezaji saba kila upande, kuvuta kamba, na pia mpira wa mezani maarufu kama fussball itapamba bonanza hilo. Burudani mbalimbali pia zitapamba bonanza hilo zikiwemo burudani ya muziki kutoka bendi ya Mastaa wa Kusini, kikundi cha sanaa cha Umoja Star au maarufu kama “Manyoka”, wacheza show wa Chicharito Group pamoja na wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wa mkoani Ruvuma.

Kalumuna pia amesema kuwa vilevile kuwa michezo mbalimbali ya kujifurahisha kama vile kufukuza kuku wa kienyeji, kukimbia na gunia na kupiga penati ukiwa umefungwa kitambaa usoni itapamba bonanza hilo ambalo ni la kwanza kufanyika katika mkoa wa Ruvuma kupitia Nani Mtani Jembe. Kampeni hii ya aina yake inatoa fursa ya kipekee kwa mashabiki hao kujumuika pamoja na kuburudika na vile vile imeongeza chachu ya ushindani na utani wa jadi kati ya mashabiki hao huku ikiwapa fursa ya kipekee kuonyesha mapenzi kwa timu zao.

Bonanza hilo linalotarajiwa kuanza saa tatu asubuhi ni mwendelezo wa kampeni ya Nani Mtani Jembe ambayo ilizinduliwa Oktoba 2 na  inafanyika nchi nzima ikiwashirikisha mashabiki wa timu kongwe za Simba na Yanga. Kupitia kampeni hiyo, Kilimanjaro Premium Lager inayozidhamini timu za Simba ya Yanga imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 na kisha kuzigawanya kwa timu hizo ambapo kila timu inazo shilingi milioni 50 ambazo zinashindaniwa na mashabiki wao.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe alisema kuwa mashabikiwa Simba na Yanga wanatakiwa kushindana kwa kushiriki kwenye kampeni hiyo ili kuhakikisha kuwa timu mojawapo inapata fedha nyingi zaidi ya timu nyingine.
Akielezea namna ya kushiriki, Kavishe alisema kuwa mpaka kila timu imetengewa shilingi milioni 50 na kuwa mshiriki wa shindano hilo la Nani Mtani Jembe ambaye ni shabiki wa Simba au Yanga anachotakiwa kufanya ni kununua bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo kwenye kizibo chake kuna namba ya kushiriki.

Alisema baada ya shabiki kununua bia ya Kilimanjaro na kuona namba ya kwenye kizibo, anachotakiwa kufanya ni kuchukua simu yake ya kiganjani na kuandika ujumbe mfupi wa maneno akianza na jina la timu anayoshabikia kisha anaandika namba iliyo kwenye kizibo na kuituma kwenye namba 15440.

Alisema baada ya shabiki kutuma namba hiyo, atakuwa amepunguza shilingi 1,000 kutoka kwa timu pinzani yaani ikiwa shabiki aliyetuma ujumbe huo ni wa Simba atakuwa amefanikiwa kupunguza shilingi 1,000 kutoka kwenye fungu la Yanga na ikiwa shabiki ni wa Yanga pia atakuwa amepunguza shilingi 1,000 kutoka kwa Simba.

Kwa mujibu wa Kavishe matokeo ya uwiano wa fedha zinavyopungua kutoka Simba au Yanga yatangazwa kila siku hadi siku ya mwisho wa shindano hilo Desemba 14, mwaka huu.

MASHABIKI WAVUNJA VITI 100, ADHABU YAINYEMELEA SIMBA - ANGALIA PICHA MECHI NA VURUGU



SEKUNDE chache kabla ya mwamuzi Mohamed Theofile wa Morogoro hajamaliza pambano la Ligi Kuu ya Bara kati ya Simba na Kagera Sugar, mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa Simba, wamevunja viti zaidi ya 100 na kuvirusha uwanjani imefahamika.
Mwandishi wa mtandao huu alishuhudia mashabiki hao wakivunja na kuvirusha uwanjani viti hivyo baada ya mwamuzi huyo kuwapa Kagera penalti iliyofungwa na Salum Kanoni.
Mashabiki hao ambao licha ya kuwa walikaa katika majukwaa tofauti, waliweza kufanya kitendo hicho kwa kile kilichoelezwa baadaye kwamba ni kupingana na maamuzi ya mwamuzi huyo.
Viti vilivyovunjwa vingi vina rangi ya chungwa na bluu ambavyo kwa haraka haraka idadi yake inaweza kuwa zaidi ya 100.
Kutokana na hali hiyo, askari wa Jeshi la Polisi walilazimika kulipua mabomu matatu ya machozi ili kuwatuliza mashabiki hao walioonekana kuwa na hasira.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura ameuambia mtandao huu kwamba, kwa kitendo hicho kamati ya mashindano na ile ya nidhamu zinaweza kukaa na kutathimini uhalibifu uliofanywa na mashabiki hao kisha timu husika kuwajibika kulipa.
“Kila mtu ameona kilichotokea na vurugu za kuvunja viti zilianza tangu wakati wa mapumziko hivyo uchunguzi utafanyika na klabu iliyohusika italipa faini kama utaratibu ulivyo,” alisema Wambura kwa kifupi.    


 Kipa wa akiba wa Simba, Abel Dhaila, akimlalamikia mwamuzi wa akiba baada ya mwamuzi wa kati kutoa penati katika dakika za majeruhi.
  Kipa wa akiba wa Simba, Abel Dhaila, na Kocha Mkuu, Abdallah Kibaden, wakimlalamikia mwamuzi wa akiba baada ya mwamuzi wa kati kutoa penati katika dakika za majeruhi.
 Wachezaji wa akiba wa Simba wakisikitika baada ya kuamuliwa kupigwa penati hiyo.
 Askari wakiendelea kumdhibiti shabiki aliyekamatwa baada ya mashabiki hao kuvunja viti na kuanza kuruka uwanjani.
Askari wakiendelea kudhibiti vurugu..
 Sehemu ya viti vilivyoharibiwa....
 Wachezaji wa Simba, wakimpongeza beki wao Salum Kanon, baada ya kusawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penati.
 Patashika langoni mwa Kagera Sugar.
 Kiungo wa Kagera Sugar, George Kavila (kulia) akimtoka mshambuliaji wa SImba, Amis Tambwe, wakati wa mchezo huo.
 Amis Tambwe, akidhibitiwa.
 Ramadhan Singano wa Simba (kushoto) akijaribu kumtoka beki wa Kagera Sugar, Malegesi Mwangwa.
 Hatari langoni mwa kagera.
 Tambwe akidhibitiwa. (PICHA ZOTE KWA HISANI YA SUFIANI MAFOTO WEBSITE)

SIMBA YAVUTWA NA KAGERA SUGAR TAIFA LEO, MABOMU YAPIGWA UWANJANI


PENALTI iliyopigwa dakika za nyongeza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliozikutanisha Simba na Kagera Sugar muda mfupi uliopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ilibadili matokeo na kufanya mchezo huo kuisha kwa sare ya bao 1-1.
Huku mashabiki wengi wakidhani mechi hiyo ingemalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, mwamuzi Mohamed Theofile wa Morogoro aliipa penalti Kagera wakati mwamuzi wa akiba akiwa ameshaonyesha dakika nne za nyongeza na mashabiki kutoamini kilichotokea.
Beki Joseph Owino ndiye aliyesababisha penalti hiyo baada ya kumchezea vibaya Daudi Jumanne wa Kagera ndani ya eneo la hatari ambapo, beki Salum Kanoni wa Kagera alifunga penalti hiyo na sekunde chache baadaye mwamuzi alimaliza pambano hilo.
Awali Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 45 lililofungwa na Amisi Tambwe baada ya mabeki wa Kagera kujichanganya katika kuokoa. Bao hilo lilidumu hadi timu hizo zilipoenda kupumzika.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi lakini hadi dakika ya 85, hakuna timu iliyoweza kupata bao kutokana na safu zote za ushambuliaji kutokuwa makini.
Mshambuliaji wa Kagera, Themi Felix pamoja na winga Paul Ngwai leo hawakuweza kufurukuta mbele ya mabeki wa Simba waliokuwa wakiongozwa na nahodha wao Nassor Masoud ‘Chollo’.
Nao washambuliaji wa Simba, Tambwe na Betram Mombeki hawakuweza kufuruka kutokana na mabeki wa Kagera kucheza kwa nguvu zaidi wakiongozwa na Maregesi Mwangwa ambaye ni nahodha wao.
Muda mfupi baada ya Kanoni kufunga bao, alienda kushangilia akiwa sambamba na wenzake mahala ambapo mashabiki wa Simba wamekaa na kuzua tafrani ya kurushiwa chupa za maji na viti vilivyovunjwa na mashabiki hao.
Kutokana na hali hiyo, askari wa Jeshi la Polisi waliokuwepo uwanjani hapo walilazimika kulipua mabomu matatu ya machozi ili kutawanya mashabiki hao, hali iliyozua hali ya taharuki uwanjani hapo.
Matokeo haya yanaifanya Simba kufikisha pointi 21 na kubaki katika nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 12.Nayo Kagera imepanda hadi nafasi ya tano ikiwa na pointi 17.

;LIVE SCORE: SIMBA SC 1 - 1 KAGERA SUGAR



Mashabiki wa Simba wanang'oa viti vya uwanja wa taifa na mashabiki wanapambana na Polisi ambao wanalipua mabomu ya machozi. 

Dk 90+5 FULL TIME! Simba 1-1 Kagera. 

Dk 90+4 GOOOOO....! Salum Kanoni anaipatia Kagera bao la kusawazisha kwa njia ya penalti. Simba 1-1 Kagera. 

Tunaomba radhi kwa uchelewaji wa updates ni kutokana na network mbovu uwanjani.

Dk 84 Tambwe anachezewa faulo na Martin Muganyizi. Simba 1-0 Kagera. 

Dk 73 Kagera wanapiga faulo na kukosa. 

Dk 73 Kipa wa Simba anachelewesha mpira na mwamuzi anaamuru faulo ipigwe kuelekea lango la Simba. Simba 1-0 Kagera. 

DK 60 Simba 1 - 0 Kagera 

Dk 57 Timu zinashambuliana kwa zamu na Kagera wanaonekana wameamka. 
Kipindi cha pili kinaanza
Dk 45 HALF TIME...! Simba 1-0 Kagera. 

Dk 45 GOOOOO...!  Simba imepata bao la kwanza kupitia kwa Amisi Tambwe ambae aliwatoka mabeki wa Kagera, Salum Kanoni na Ernest Mwalupani. 

DK 40 Simba wanalisakama lango la Kagera wakisaka goli. Ila milango bado ni migumu.

DK 30' Simba 0-0 Kagera Sugar 

Dk 21 Kagera wamefanya mabadiliko ya kipa, katoka agaton anthony ambaye ameumia bada ya kugongana na Tambwe kaingia hannington kalyesubula. 

DK 10 - Simba 0-0 Kagera Sugar

DK 5 Timu zinacheza soka taratibu kwa kusomana

Dk 00 MPIRA UMEANZA! 

Simba: Abuu Hashimu, Nassoro Masoud 'Chollo', Issa Rashid, Joseph Owino, Hassan Khatib, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Said Ndemla, Betram Mwombeki, Amisi Tambwe na William Lucian

Kagera Sugar: Agaton Antony, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Ernest Mwalupani, Malegezi Mwangwa, Zuberi Dabi, Benjamin Asukule, George Kavilla, Themi Felix, Daudi Jumanne na Paul Ngwai

Wednesday, October 30, 2013

SIR ALEX FERGUSON AVUNJA REKODI NYINGINE - MAUZO YA KITABU CHAKE YAFUNIKA

Hot cakes: Fergie's book has been a quick seller
Hot cakes: Fergie's book has been a quick seller
REUTERS
Kitabu cha Sir Alex Ferguson kimeweka rekodi ya kuwa kitabu kilichooza kwa haraka zaidi ndani ya Uingereza kikiuza nakala 115,547 katika siku chache za mauzo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka The Bookseller, kitabu hicho cha mocha wa zamani wa Manchester United kimevunja rekodi ya  Delia Smith,  ambaye kitabu chake cha mwaka 1999 cha mapishi kiliuza kopi 112,000 katika wiki take ya kwanza.

Pia kitabu cha Fergie kimevunja rekodi ya mauzo ya kitabu cha rafiki yake waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair, ambacho kiliuza kopi 92,000 katika wiki ya kwanza.

VITABU VILIVYOUZA ZAIDI UK:
Sir Alex Ferguson - My Autobiography - 115,547
Delia Smith - How to Cook - book two - 112,000
Tony Blair - A Journey - 92,000
David Beckham - My Side - 86,000
Paul Burrell - A Royal Duty - 77,000

SIMBA KURUDISHA MAKALI YAKE KESHO DHIDI YA KAGERA SUGAR???


SIMBA, KAGERA SUGAR KUUMANA KESHO
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaanza raundi ya 12 kesho (Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Viingilio katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kupitia TBC 1 vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A.

Nayo Yanga itashuka uwanjani Novemba Mosi mwaka huu katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.

Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

PAMBANO LA YANGA, MGAMBO SHOOTING LAINGIZA MIL 37/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Mgambo Shooting lililochezwa jana (Oktoba 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 37,915,000.

Washabiki waliohudhuria mechi hiyo namba 46 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 walikuwa 6,515 ambapo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 5,783,644.07, gharama za kuchapa tiketi sh. 3,145,790 wakati kila klabu ilipata sh. 8,550,741.95.

Wamiliki wa uwanja walipata sh. 4,347,834.89, gharama za mchezo sh. 2,608,700.93, Bodi ya Ligi sh. 2,608,700.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,304,350.47, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,014,494.81.

URAISI WA TFF - RAISI WA CAF ISSA HAYATOU AMPONGEZA JAMAL MALINZI


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou amempongeza Jamal Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Katika salamu zake kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya CAF na familia ya mpira wa miguu Afrika, Rais Hayatou amesema uchaguzi huo unampa Rais Malinzi fursa ya kuupeleka mbele mpira wa miguu nchini Tanzania.

Amesema CAF ina imani uwezo wake katika uongozi, uzoefu na ujuzi katika mpira wa miguu havitausaidia mpira wa miguu Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla, na kuongeza kuwa ataendeleza ushirikiano uliopo ili kuwanufaisha zaidi vijana wa bara hili.

Rais Hayatou amemtakia Rais Malinzi kila la kheri katika kipindi chake cha uongozi na kumhakikishia kuwa CAF iko pamoja naye katika kusukuma mbele gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu.


Tuesday, October 29, 2013

FIFA YATOA MAJINA YA WANASOKA WANAOWANIA TUZO YA MWANASOKA BORA WA DUNIA.



YANGA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU - YAIPIGA MGAMBO 3-0


Kikosi cha Young Africans kilichoanza dhidi ya Mgambo Shooting


 Young Africans mabingwa mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara leo wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa timu ya Mgambo Shooting kutoka mkoani Tanga kwa mabao 3-0, mchezo uliofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Ikiwa na kumbukumbu ya ushindi katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Rhino Rangers kwa mabao 3-0, kikosi cha Young Africans kiliingia uwanjani kwa lengo la kuendeleza wimbi la ushindi na ndivyo hali ilivyokuwa

Hamis Kiiza, Saimon Msuva na Mrisho Ngasa walikosa mabao ya wazi dakika 15 za kipindi cha kwanza kufuatia kutokua makini katika umaliziaji na kujikuta mipira yao ikitoka pembeni mwa lango la Mgambo Shooting na mingine ikiokolewa na golikipa wa Mgambo Shooting Tonny Kavishe.

Mbuyu Twite aliipatia Young Africans bao la kwanza Young Africans dakika ya 31 ya mchezo kwa shuti kali la mita 25 kwa mpira wa adhabu alioupiga na kujaa moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe kwa washabiki wa Yanga.

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Young Africans 1 - 0 Mgambo Shooting.

Kipindi cha pili kilianza kwa Young Africans kufanya mabadiliko ambapo aliingia nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' kuchukua nafasi ya Rajab Zahir mabadiliko ambayo yaliongeza uwezo wa kumiliki mchezo na kulinda vyema lango lao.

Dakika ya 50 ya mchezo, Hamis Kiiza 'Diego' aliipatia Young Africans bao la pili kwa mkwaju wa penati kufuatia mlinda mlango wa Mgambo Shooting Tony Kavishe kumuangusha Didier Kavumbagu ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru ipigwe penati ambayo Kiiza hakufanya makosa.

Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao tatu la mchezo dakika ya 67 ya mchezo baada ya mpira uliorushwa na mlinzi Mbuyu Twite kumkuta Kavumbagu ambaye aliwazidi maarifa walinzi wa Mgambo Shooting na kuukwamisha mpira wavuni.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 3 - 0 Mgambo Shooting.

Msimu uliopita katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom uliofanyika kati ya timu hizi Young Africans pia iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, mabao yaliyofungwa na Didier Kavumbagu, Jerson Tegete na Nadir Haroub 'Cannavaro' 

Young Africans: 1.Dida, 2.Twite 3.Oscar, 4.Rajab/Cannavaro 5.Yondani, 6.Chuji, 7.Msuva/Lusajo 8.Domayo, 9.Kavumbagu, 10.Ngassa, 11.Kiiza

BAHATI MGUNGA- ''UMUHIMU WA KUWA NA VILABU IMARA,VIONGOZI WA MIKOA IMARA''.




Monday, October 28, 2013

TEGETE NI MFUNGAJI MZURI BADO ILA AMEKOSA UMAKINI TU


Na Baraka Mbolembole
" Ni kweli sisi wachezaji tunajua kuwa mashabiki wanazipenda timu zao, hasa kwa wale wa timu yetu ya Yanga tunajua wanaipenda sana timu yao, lakini nawashauri wabadilike sasa, wasiwazomee wachezaji wakati wanapokuwa wanafanya vibaya. Wawe na subira kama kweli wanaipenda timu yao. Kelee zao huwatoa mchezoni wachezaji na kujikuta wakifanya vibaya zaidi, na hili hupelekea hata kwa wale wachezaji wanaokuja kuingia katika uoga, nawasihi wawe na uvumilivu"
Ni maneno ya mshambuliaji aliye katika wakati mgumu hivi sasa katika klabu ya Yanga, Jerry Tegete, wakati nilipofanya nae mazungumzo hivi karibuni kuhusiana na mwenendo wake usiovutia hadi sasa katika klabu hiyo.

Jerry ambaye alianza vizuri msimu huu pale alipofunga maba mbili siku ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Ashanti United, na akafunga tena katika mchezo uliofuata hila amekuwa akipoteza nafasi za wazi mara kwa mara na kupelekea ,kuwakera wengi.
Wakati ushindani wa kuwania nafasi ukiwa ni mkubwa katika safu ya mashambulizi ya Yanga, ambayo imekusanya washambuliaji sita wa kati na wengine wawili wakiwa kama viungo washambuliaji, Jerry amejikuta akipoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza, na katika siku za karibuni amekuwa akikosa hata nafasi ya kuingia kama mchezaji wa akiba.

Didier Kavumbagu, ameoneka kuwa chaguo la kwanza mbele ya kocha, Ernie Brandts, na Mrundi huyo ameweza kuwa kiongozi wa safu yote ya mashambulizi, nguvu, akili na uwezo wa kumiliki mpira, unaambatana na umakini mkubwa wa kutumia nafasi anazotengenezewa, ' Kavu' amekuwa chaguo bora mbele ya Tegete katika vitu vingi, mwanzoni mwa msimu walipangwa walikuwa wakipangwa pamoja na wakaonekana kuwa wafungaji wazuri, walifunga kwa vichwa, na uwezo binafsi na matokeo yake wakawa chaguo la kwanza.
" Ushindani ni mkubwa sana, na nafasi imekuwa ni ngumu, kila mchezaji hutumia nafasi anayopata vizuri" anaongeza, Tegete. 'Kavu', Tegete, Said Bahanunzi, Hussein Javu, Kondo awali walikuwa washindani wa kwanza katika nafasi hii, ila kurejea kwa Hamis Kizza aliyekuwa kwenye majaribio nchi ya ng'ambo, na kumalizika kwa adhabu ya Mrisho Ngassa kumefanya hali ya mambo kuwa magumu zaidi.
Lakini inakuwaje kwa mchezaji kama Jerry kuzomewa mara kwa mara na mashabiki wa timu yake? Wakati fulani hali hii iliwahi kumtokea kiungo wa zamani wa timu hiyo, Nurdin Bakari, hasa pale alipokuwa akifanya vibaya uwanjani, kila mtu alikuwa anafahamu uwezo wake, lakini pasi mbili au tatu tu ' mbovu' uwanjani zilikuwa ni tatizo. Kitu kizuri huleta furaha ya siku zote katika maisha, ni shida sana kukishusha chini kitu kizuri, mafanikio hayahitaji kubweteka na kupelekea mtu kujisahau kule alipotoka na alipokuwa amepanga kufikia, umakini, nidhamu ya mchezo, huwa ni sehemu ya mipango mizuri ya wachezaji wote waliofanikiwa. Wapo ambao walipitia njia ya kupingwa na kuzomewa na mashabiki wa timu zao ila bado wakafanya kazi nzuri uwanjani na kujikuta wakifanikiwa.

Dr. Martin Luther King Jr aliwahi kusema; " Ukimya wa rafiki yako unaumiza sana kuliko kelele za adui yako" pengine, manaharakati huyu wa haki za binadamu, na aliyekuwa mtetezi wa watu weusi katika Marekani, alikuwa na maana nyingi lakini ni vyema wakati mwinmgine wachezaji kama Tegete wakachukulia kelele za zomea zomea za mashabiki wao ni sehemu za kuwakumbusha kuwa hawafanyi vizuri. Na mashabiki hawatakiwi kufanya hivyo mara kwa mara klwa kuwa mara moja au mbili inatosha kufikisha ujumbe kwa muhusika.

Katika miaka mitatu ya karibuni, Tegete amekuwa akikumbwa na majeraha ya mara kwa mara, na hajawahi kucheza michezo sita mfululizo ndani ya misimu mitatu sasa klabuni kwake.
" Namshukuru Mungu kwa kila jambo, nashukuru hivi sasa nimepona goti, hilo ndilo lilikuwa ni la muhimu sana kwangu. Unajua hata sisi wachezaji hatupendi kufanya vibaya, wakati wa mchezo na Simba niliumia na kusikitika sana kwa sababu hadi nusu ya kwanza tunaongoza 3-0, kipindi cha pili wakarudisha goli zote.

Niliumia sana goli kurudi na nilikuwa nina imani tungeweza kuongeza bao lingine muda wowote. Simba walijitahidi sana" . Hili ni kweli kuwa hakuna mchezaji anayependa kufanya vibaya na wakati mweingine matokeo yao mabaya uwanjani hutokana na uwezo mzuri wa timu nyingine. Ila mimi binafsi nahitaji mabao kutoa kwa Tegete, nimechoka kumuona akipoteza nafasi rahisi mara kwa mara mchezoni, ila ujumbe wangu kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba, ' Muacheni, Jerry acheze mpira sasa, baaada ya kucheza walau michezo mitao hadi saba mfululizxo mnaweza kumuhukumu' . Tegete ni mfungaji mahiri bado, amekosa umakini tu kama aliona nao Kizza au Kavumbagu.
0714 08 43 08

YANGA, MGAMBO JKT KUVAANA TAIFA LEO

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Bara leo itashuka katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kupambana na Mgambo JKT katika mchezo wa raundi ya kumi na moja ya ligi hiyo.

Yanga inaingia uwanjani leo ikiwa na pointi 19 ilizopata katika mechi 10 ilizocheza huku ikiwa nafasi ya nne. Azam inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 23 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 20 huku zote zikiwa zimecheza mechi 10. Mbeya City ni ya tatu ikiwa na pointi 20 katika mechi 10.

Kwa upande wao, Mgambo wanaingai uwanjani wakiwa na pointi tano walizopata katika mechi 10. Timu hiyo inaburuza mkia katika ligi hiyo.
Kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya leo kutakuwa mchezo utakaozikutanisha timu mwenyeji za mkoa huo ambazo ni Mbeya City na Tanzania Prisons. Rhino Rangers na JKT Ruvu zitacheza katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Raundi ya 12 ya ligi hiyo itaanza Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Novemba Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu kwenye uwanja huo huo.
Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.

Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

MSIMAMO WA LIGI KUU YA VODACOM BAADA YA AZAM KUISURUBU SIMBA



KIBADENI AKUBALI YAISHE, MALARIA YAIPONZA SIMBA


MUDA mfupi tu baada ya timu yake kufungwa mabao 2-1 na Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni, amesema, “Nakubali tumefungwa kwa haki na ni moja ya sehemu ya mchezo.”
Kibadeni amesema kiukweli mabao yote ya Azam yalitokana na makosa waliyofanya lakini amewasifu vijana wake kuweza kucheza vizuri hasa kipindi cha kwanza japokuwa wamefungwa. Hii ni mara ya kwanza Simba kufungwa katika msimu huu wa ligi ikiwa chini ya Kibadeni.
“Nakubali matokeo haya, nadhani wote mmeona jinsi mpira ulivyochezwa, wenzetu wametumia makosa yetu na kupata ushindi. Katika soka ukipata nafasi ya kufunga unatakiwa kufanya hivyo kama walivyofanya Azam, sasa tunajiandaa na mchezo ujao,” alisema Kibadeni.
Naalipoulizwa kutokuwepo kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kama mabeki Gilbert Kaze na Nassor Masoud ‘Chollo’ ambao nafasi zao zilichezwa na William Lucian ‘Gallas’ na Hassan Khatib, Kibadeni alijibu; “Wachezaji hao ni wagonjwa, Kaze anaumwa malaria kama ilivyo kwa Chollo ndiyo maana leo hamjawaona uwanjani.
“Kiasi fulani kukosekana kwao kumeifanya mechi hii kuwa ngumu kidogo maana hawa vijana bado wadogo wanaohitaji muda kuweza kumudu michezo mikubwa kama hii.”
Kibadeni pia hakumchezesha mshambuliaji Amisi Tambwe ambaye hadi sasa anaongoza kwa ufungaji katika ligi hiyo akiwa amefunga mabao nane, akifuatiwa na Hamisi Kiiza wa Yanga, Juma Liuzio wa Mtibwa na Elius Maguri wa Ruvu Shooting ambao wote wana mabao saba.
Kocah huyo alisema, hakuweza kumpanga Tambwe kutokana na kuwa majeruhi wa goti lakini anaweza kucheza mechi ijayo endapo afya yake itaimarika ndani ya saa 72 zijazo.
Ushindi huo wa Azam unaifanya timu hiyo kuishusha Simba kileleni mwa ligi hiyo na kuketi yenyewe ikiongoza kwa pointi 23 ilizopata baada ya kucheza mechi 11 kama ilivyo kwa Simba ambayo inapoteza mechi yake ya kwanza tangu kuanza kwa ligi hii msimu huu.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 20 ilizopata baada ya kucheza mechi 11, ambapo imeshinda mechi tano na kutoka sare tano. Simba imefunga mabao 21 na kufungwa mabao 10.
Katika mchezo wake ujao, Simba itacheza na Kagera Sugar Oktoba 31 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Azam ikipambana na Ruvu Shooting Novemba 2 mwaka huu kwenye Uwanaj wa Azam Complex, Dar es Salaam.

AZAM YAIPIGA SIMBA 2-1, YATIBUA REKODI YA MNYAMA, KIPRE TCHETCHE AFUNGA BAO LA MWAKA



BAO lililofungwa dakika ya 73 na mshambuliaji Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast limeiwezesha Azam FC kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tcheche alifunga bao hilo akiwa wingi ya kushoto ya uwanja huo na alipiga shuti kali la chinichini akiwa pembeni mwa uwanja (impossible angle) na mpira kutinga wavuni moja kwa moja. Kipa Abel Dhaira wa Simba pengine alidhani mfungaji alipiga mpira huo kama krosi kwenda kwa John Bocco, hivyo hakuwa makini kuzuia mpira huo wa kwanza.
Awali Tchetche alikuwa amepokea pasi kutoka kwa Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ kutoka katikati ya uwanja. Sure Boy alipokea pasi baada ya mshambuliaji wa Simba, Betram Mombeki kupokonywa mpira jirani na katikati ya uwanja.
Ushindi huo wa Azam unaifanya timu hiyo kuishusha Simba kileleni mwa ligi hiyo na kuketi yenyewe ikiongoza kwa pointi 23 ilizopata baada ya kucheza mechi 11 kama ilivyo kwa Simba ambayo inapoteza mechi yake ya kwanza tangu kuanza kwa ligi hii msimu huu.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 20 ilizopata baada ya kucheza mechi 11, ambapo imeshinda mechi tano na kutoka sare tano. Simba imefunga mabao 21 na kufungwa mabao 10.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ dakika ya 22 akimalizia pasi safi ya Zahor Pazi na kuamsha furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilionekana kutawala mchezo lakini Azam walizinduka kuanzia dakika ya 35 na kulishambulia lango la Simba kama nyuki na kufanikiwa kupata bao dakika ya 43 mfungaji akiwa ni Tchetche aliyemalizia kazi nzuri ya beki Erasto Nyoni.
Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko matokeo yalikuwa ni bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kufanya mabadiliko ambapo walimtoa beki Said Moradi na nafasi yake kuchukuliwa na David Mwantika ambaye aliweza kupunguza kasi ya mashambulizi ya Simba kwa kiasi fulani.
Dakika 10 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko baada ya kuwatoa kwa mpigo Zahor Pazi na Amri Kiemba na nafasi zao kuchukuliwa na Sino Augustino na Edward Christopher.
Mabadiliko hayo hayakuweza kuisaidai Simba licha ya mara kadhaa kufika langoni kwa Azam lakini washambuliaji wake Sino Augustino na Mombeki hawakuwa makini kumalizia mipira mingi waliyokuwa wakipewa na viungo.
Tatizo la ukabaji wa nafasi ndilo lililoigharimu Simba na kumfanya Tchetche aifungie Azam bao la pili dakika ya 73.
Katika mchezo wake ujao, Simba itacheza na Kagera Sugar huku Azam ikipambana na Ruvu Shooting.

LIVE SCORE: SIMBA SC 1-2 AZAM FC FULL TIME



Dk 90+4 FULL TIME! Simba 1-2 Azam. 

Dk 90 Bocco anapiga shuti kali kuelekea lango la Simba lakini mpira unatoka juu ya lango. Muda wowote mpira unaisha. Simba 1-2 Azam. 

Dk 82 Mombeki anamchezea rafu Sure Boy. 

Dk 80 Manula ananyanyuka baada ya kutibiwa na mpira unaendelea. 

Dk 78 Kipa wa Azam, Aishi Manula anagongana na Sino Augustino wa Simba na anaumia. Mpira unasimama kwa muda ili atibiwe. 

Dk 77 YELLOW CARD..! Sure Boy anaonyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Singano wa Simba. 


Dk 75 Morris anamchezea rafu Betram Mombeki. 

Dk 74 SUB: Azam imefanya mabadiliko ametoka Humphrey Mieno ameingia Khamis Mcha. 

Kipre Balou anafunga bao la pili kwa upande wa Azam - ni goli la uzembe wa kipa Abel Dhaira.

Dk 69 YELLOW CARD...! Hassan Khatib wa Simba anaonyeshwa kadi ya njano baada ya kumchzea rafu Tchetche rafu. 

Dk 68 Simba inapata kona lakini Azam wanaokoa. 

Dk 67 YELLOW CARD...! Aggrey Morris wa Azam anaonyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea vibaya Edward Christopher wa Simba. 

Dk 63 John Bocco wa Azam anakosa bao la wazi akishindwa kumalizia pasi nzuri ya Tchetche. Simba 1-1 Azam. 

Dk 55 SUB: Simba inafanya mabadiliko wametoka Amri Kiemba na Zahor Pazi na nafasi zao zimechukuliwa na Sino Augustino na Edward Christopher. 

Dk 48 SUB: Azam ilimtoa Said Moradi akaingia David Mwantika.

Dk 47 Azam wametawala kiungo na wanafanya mashambulizi mengi langoni kwa Simba. 

Dk 45 KIPINDI CHA PILI KIMEANZA! 

Mpira ni mapumziko Simba 1 - 1 Azam FC

Dk 43' Simba 1-1 Azam Kipre Tchetche anaisawazishia Azam FC na kwenda kushangilia na mashabiki wa Yanga.  

DK 30 - Simba wanaendelea kuongoza kwa bao moja bila.

DK 21' Goooooo Simba 1- 0 Azam .Ramadhan Singano anaishangaza Azam

Dk 15 Simba 0-0 Azam

Dk 8'  Zahoro Pazi anafunga goli lakini mwamuzi analikataa na anapewa kadi ya njano. 

DK 1' Azam wanapata free kick inapigwa vibaya na John Bocco Simba 0-Azam 

Kikosi cha Azam FC
Mwadini Ally
Erasto Nyoni
Waziri Salim
Said Moradi
Aggrey Morris
Kipre Bolou
Salum Abubakar
Humphrey Mieno
John Niccolo
KipreTchetche
Joseph Kimwaga

MAJERUHI SIMBA HADI MWEZI UJAO


Viungo wawili chipukizi wa timu ya soka ya Simba, Abdallah Seseme na Ibrahim Twaha wataendelea kuuguza majeraha yao hadi baadae mwezi ujao. Seseme bado anauguza majeraha ya kuvunjika vidole viwili vya mwisho, wakati Twaha aliyesajiliwa msimu huu akitokea timu ya Coastal Union anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
Wakisema hayo kwa nyakati tofauti wakati walipozungumza na mtandao huu viungo hao wamekiri kuwa hawana nafasi ya kurejea tena uwanjani katika michezo ya mzunguko wa kwanza.
" Niliumia vidole viwili vya mwisho vya mguu wa kushoto wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Lipuli. Mguu ulikleki sasa nimewekewa P.O.P hadi mweizi ujao. Nina miezi miwili sasa bado nauguza majeraha haya" anasema Seseme
Kwa sasa nipo katika uchunguzi kama nimechanikla au ni maumivu ya kawaida tu. Nimeumia nyama za paja la mguu wa kulia" anasema Twaha ambaye amecheza michezo mitatu ya timu yake huku akikosa michezo miwili ya mwanzo ya msimu huu kwa kuwa timu yake ya zamani ilimuwekea pingamizi.
Simba itacheza na timu ya Azam FC katika mchezo wa raundi ya 11 ya ligi kuu wakijaribu kutanua wigo la pointi katika kilele cha msimamo.

JAMAL MALINZI AVUNJA KAMATI ZOTE ZA TFF - ATOA MSAMAHA KWA WALIOFUNGIWA



Jamal Emil Malinzi ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Malinzi ameshinda wadhifa huo katika uchaguzi wa Kamati ya Utendaji ya TFF uliofanyika juzi (Oktoba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Aliibuka na ushindi wa kura 73 dhidi ya mpinzani wake pekee Athuman Jumanne Nyamlani aliyepata kura 52. Nafasi ya Makamu wa Rais imetwaliwa na Wallace Peter Karia aliyepata kura 67 na kuwashinda Ramadhan Omari Nassib kura 52 huku Imani Omari Madega akipata kura sita.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Rais Malinzi ametaka ushirikiano kutoka kwa wadau wote akiwemo mpinzani wake Nyamlani katika kuhakikisha mpira wa miguu nchini unasonga mbele.

Pia ametoa msamaha kwa watu wote waliokuwa wamefungiwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na TFF. Msamaha huo hauwahusu wale waliofungiwa kwa makosa ya rushwa au kupanga matokeo. Vilevile msamaha huo hauhusu adhabu zilizotolewa katika ngazi ya klabu.

Rais Malinzi pia amevunja kamati zote za TFF ambapo ataziunda upya kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji.

Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera) aliyepata kura 102 za ndiyo na 17 za hapana. Kanda namba 2- Mara na Mwanza, mshindi ni Vedastus Lufano aliyepata kura 51 dhidi ya Jumbe Odessa Magati (11), Mugisha Galibona (24), na Samwel Nyalla (39).

Epaphra Swai ndiye mshindi wa Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu kwa kura 63 dhidi ya Mbasha Matutu aliyepata 61. Kanda namba 4- Arusha na Manyara mshindi ni  Omali Walii Ali aliyepata kura 53 dhidi Elley Mbise (51), Ally Mtumwa (19).

Kanda namba 4- Kigoma na Tabora, mshindi ni Ahmed Idd Mgoyi aliyepata kura 92 dhidi ya 28 za Hamisi Yusuf Kitumbo.

Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo ameshinda Kanda namba 6- Katavi na Rukwa kwa kura 73 dhidi ya Ayubu Nyaulingo aliyepata 52. Ayoub Shaibu Nyenzi ndiye mshindi wa Kanda namba 7- Iringa na Mbeya kwa kupata kura 59 na kuwapiku David Samson Lugenge (8), John Exavery Kiteve (12) na Lusekelo Elias Mwanjala (46).

Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma inawakilishwa na James Patrick Mhagama aliyepata kura 93 dhidi ya 31 za Kapteni mstaafu Stanley William Lugenge. Athuman Kingombe Kambi ndiye mshindi wa Kanda namba 9- Lindi na Mtwara kwa kura 84 akiwazidi Francis Kumba Ndulane (30) na Zafarani Mzee Damoder (11).

Hussein Zuberi Mwamba ametetea ujumbe wa Kanda namba 10- Dodoma na Singida kwa kura 63 akiwapiku Stewart Masima (58) na Charles Komba (4). Geofrey Irick Nyange ameshinda Kanda namba 11- Morogoro na Pwani akipata kura 78 dhidi ya Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na Twahil Twaha Njoki (2).

Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani, Khalid Abdallah Mohamed ndiye aliyeibuka kidedea kwa kura 69 dhidi ya 54 za mpinzani wake Davis Elisa Mosha. Kidao Wilfred Mzigama ameshinda Kanda namba 13- Dar es Salaam kwa kupata kura 60 dhidi ya wapinzani wake Muhsin Said Balhabou (50), Omar Isack Abdulkadir (10) na Alex Crispine Kamuzelya (4).

HOTUBA YA KWANZA YA JAMAL MALINZI,RAISI MPYA WA TFF

 Hatimaye Tumechagua Mabadiliko,
Salamu kwa wanafamilia wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Salamu kwa wapenda michezo wa ndani na nje ya nchi yetu Tanzania.

Naanza kwa kumshukuru Mungu kwa hekima, busara, akili, vipaji na uwezo aliotujaalia kutuwezesha kutenda yote haya kwa amani na utulivu.

Shukrani za dhati zimwendee Bw. Leodegar Tenga, rais wa TFF 2005 - 2013 anayekabidhi madaraka kwa rais mpya wa TFF. Yeye na timu yake kwa hakika wanastahili pongezi kwa mengi mazuri waliyofanya.

Shukrani kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi 2013 kwa kunikubali, mimi Jamal E. Malinzi niwe Rais wa TFF kwa kipindi kijacho cha miaka minne.

Kweli dunia imekuwa kijiji, kwani kipindi cha masaa 72 baada ya kuzindua ilani yangu ya uchaguzi, nimepokea salamu, maoni na mapendekezo toka ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Burundi, Ivory Coast, Denmark na NewZealand.

Kupitia www.jamalmalinzi.com, twitter @jamalmalinzi, Jamii Forum, Facebook na mitandao mingine, naomba tuendelee kuwasiliana, kutoa maoni, kukosoa na kuchangia mijadala yenye tija na ufanisi ili Tanzania yote ipate neema ya mpira wa miguu.

Safari ni ndefu na wasafiri ni wengi kwenye vyombo vichache vya usafiri. Kwa wale ambao tayari wana ramani ya safari yetu, sote bila kujali tofauti zetu hasa wakati wa kuwania uongozi, tutoe mchango wake ili Tanzania isonge mbele katika ulimwengu wa soka.

Naam, kuna msemo wa Kiswahili unaosema 'kukata tamaa ukingali unaishi ni dhambi'. Naomba msemo huu na utuongoze kila tunapojikwaa tunanyuke na kuendelea na safari hadi tufike tulipopakusudia.

Historia imeshaanza kuandikwa, mwaka 2013 ni Tumechagua Malinzi, Tumechagua Mabadiliko na sasa tunasonga mbele.
Jamal E. Malinzi
Oktoba 27, 2013

Sunday, October 27, 2013

MALINZI AMBWAGA KWA MBALI NYAMLANI, WALLACE KARIA AMTOA RAMADHAN NASIB


RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga usiku wa kuamkia leo amemtangaza rasmi Jamal Malinzi kuwa rais mpya wa Shirikisho hilo baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa TFF kwenye Ukumbi wa NSSF Waterfront, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa, Malinzi alipata kura 73, huku mpinzani wake pekee Athuman Nyamlani akiambulia kura 52. Hii ni tofauti ya kura 21 kati ya mshindi Malinzi na Nyamlani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ndiye aliyetangaza matokeo hayo na kuamsha shangwe ukumbini hapo huku wapambe wa wagombe wengine wakitoka vichwa chini.
Awali kabla ya uchaguzi huo, Nyamlani ndiye aliyekuwa Makamu wa rais wa TFF.
Kwa upande wa makamu wa rais wa TFF, aliyeshinda ni Wallace Karia aliyepata kura 67, akifuatiwa na Ramadhan Nasib aliyepata kura 52 na Iman Madega aliyepata kura 6 tu.
Kabla ya uchaguzi huo, Karia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi inayoendesha Ligi Kuu ya Bara na Ligi Daraja la Kwanza.
KIDAU, MGOYI, KABURU, NYENZI WASHINDA UJUMBE
Katika uchaguzi wa wajumbe wa kamati ya utendaji, Wilfred Kidau alishinda kwa upande wa kanda ya Dar es Salaam akiwabwaga Alex Crispine Kamuzelya, Muhsin Said Balhabou na Omary Isack Abdulkadir. Aliyeshinda kanda ya Pwani na Morogoro ni Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliyewabwaga Farid Nahdi, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala na Twahil Twaha Njoki.
Khalid Mohamed ameshinda ujumbe kanda ya Tanga, Kilimanjaro akimshinda Davis Elisa Mosha. Naye Msafiri Mgoyi ameshinda kanda ya Tabora na Kigoma akimshinda Yusuf Hamis Kitumbo. Ayoub Nyenzi ameshinda kwa upande wa Iringa na Mbeya akiwashinda David Lugenge, John Exavery Kiteve, na Elias Mwanjala.
Kwa upande wa Ruvuma na Njombe aliyeshinda ni James Mhagama aliyemshinda Stanley William Lugenge. Naye Athuman Kambi ameshinda kanda ya Lindi na Mtwara akiwashinda Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder. Na Blassy Kiondo ameshinda kanda ya Katavi, Rukwa akimbwaga Ayubu Nyaulingo
Categories:

0 comments:

Post a Comment

    Blogger news

    Blogroll

    Pages

    About