KWA UFUPI
Wasomi wengi ambao wameajiriwa, walinieleza kuwa wanafanya kazi zao kwa juhudi na maarifa ili kupandishwa madaraja na kupata mishahara mikubwa itakayowaweza kupata maisha mazuri.

umewahi kutamani kuwa tajiri? Siku zote ninapojaribu kuwauliza swali hili watu ninaokutana nao, hugundua kuwa karibuni kila mtu anapendelea kuwa tajiri. Kila mtu hutamani utokee muujiza apate utajiri.
Wengine, hasa wafanyakazi wanahangaika usiku na mchana kutafuta mtaji utakawawezesha kuanza biashara na kupata utajiri. Jambo linalonishangaza ni kuwa watu wanaonieleza wanataka utajiri huwa wana hali tofauti za kimaisha.
Wengine huwa na maisha mazuri na wana karibu kila kitu ambacho mtu angekihitaji ili kuwa na maisha mazuri. Kuna wengine ambao kwa hakika huwa na hali mbaya, hata chakula cha siku huwa shida. Jambo hili lilinifanya niulize swali jingine; Je, tunaposema utajiri maana yake ni nini?
Je utajiri ni nini?
Baada ya kuuliza swali kama watu wanataka utajiri au hapana niliuliza swali jingine. Nilitaka wanieleze maana ya utajiri wanaoutaka. Nilipata majibu mengi ambayo ilinibidi niyachambue na kueleza kwa muhtasari kama ifuatavyo:
“Utajiri ni hali ya mtu kuwa na fedha nyingi zitakazomwezesha kupata kitu chochote anachohitaji au huduma yoyote anayotaka duniani. Hii ni pamoja na kuwa na nyumba nzuri yenye mazingira ya kuvutia na kuwa na vitu, zana na vifaa vyovyote ambavyo mtu anavihitaji yeye na familia yake ili awe na maisha ya fuhara, starehe na anasa. Aidha awe na uwezo wa kuwalea watoto wake vizuri kwa kuwapia chakula mavazi na malazi bora pamoja na huduma muhimu za hali ya juu katika elimu afya na burudani. Aweze kwenda kokote duniani na kukutana na mtu yeyote ambaye angeona fahari kukutana naye na kuongea naye.
Pia kuwa na uwezo wa kuilea familia na ndugu zake na kusaidia jaama wenye shida. Licha ya kuwa na vitu vinavyoonekana, awe na uwezo wa kuhakikisha amani na usalama wake na familia yake, pia kuwa na tahadhari ya kifedha kwa ajili ya matukio yoyote yanayoweza kumfika binadamu.
Kuna mmoja alisisitiza kuwa mali inahitaji ulinzi na usalama wa hali ya juu kwa sababu inaweza kuwa chanzo cha wasiwasi na mashaka yanayoweza kufanya maisha yasiwe ya furaha.
Nakumbuka mzee wa zamani aliyekuwa na ng’ombe karibu 1000 na fedha nyingi alizoziweka kwenye madebe na kuzifukia katika sakafu ya nyumba yake.
Usiku ulipoingia ulikuwa mtihani. Ilikuwa lazima yeye mwenyewe na walinzi wake wakeshe usiku kucha huku wameshika bunduki zao wakilinda ng’ombe wasiibiwe. Fikiria utajiri wa mzee huyu waliokuwa wakimwita ‘tajiri ng’ombe’ kama ulikuwa na furaha. Badala ya mali yake kumtunikia yeye na kumpa starehe ilibadilika kuwa kero. Yeye anaitumikia na imemfanya kuwa mtumwa.
Je, mtu afanye nini ili kuwa tajiri?
Baada ya kujua kuwa watu wengi wanapenda kuwa matajiri niliwauliza wanafikiria kufanya nini ili kupata utajiri. Nilipigwa butwaa kugundua kuwa wengi walikuwa wanatumaini siku moja bahati itawaangukia na kuwawawezesha kupata fedha zitakazowasaidia kupata mali. Wale waliokuwa na hali mbaya zaidi waliniambia kuwa wao wanaomba siku moja utokee muujiza utakaowawezesha kupata utajiri.

0 comments:

Post a Comment

    Blogger news

    Blogroll

    Pages

    About